Ifahamu Sports Massage

Sports Massage – Massage ya Michezo

Massage ya michezo ni unyumbulishaji wa kitaalamu wa tishu laini za mwili ambapo huzingatia misuli inayohusiana na mchezo fulani. Wataalamu wa massage hutumia mbinu mbalimbali za kimijongeo kama vile ukandaji (kneading), ubonyezaji, usuguaji, mtetemo (vibration)  na unyooshaji (stretching).

 

Mbinu hizi za kimjongeo zinazofanywa na wataalamu wa Massage zinalenga kuuwezesha mwili wa mwanamichezo kuweza kufikia ufanisi wa hali ya juu katika mchezo, kuuweka mwili fiti, kupunguza uwezekano wa kupata jeraha pamoja na (au) kusaidia jeraha kupona kwa haraka. 

 

Massage ya michezo inafanywa kabla ya mchezo kwa ajili ya kuuweka mwili fiti au wakati wa mchezo kwa ajili ya kuimarisha mwili wa mwanamichezo na baada ua mchezo kwa ajili ya kuiweka misuli sawa pamoja na kuondoa uchovu.

 

Tafiti nyingi zilizofanywa ikiwemo na tafiti iliyofanywa na Frontiers in Physiology mwaka 2018 inaonyesha kwamba massage ya michezo inaongeza ufanisi kwa mwanamichezo pamoja na kuuweka mwili wake fiti.

 

Zifuatazo ni faida za Massage ya Michezo.

  1. Huimarisha misuli na kuiweka tayari kwa ajili ya mchezo: Massage husaidia kuondoa ukakamavu wa misuli na kuifanya iwe laini na yenye ufanisi, hivyo humpa nguvu mchezaji ya kukabiliana na mchezo au mazoezi.

 

  1. Huondoa maumivu katika misuli: Massage ya michezo inaondoa maumivu yaliyopo katika misuli baada ya mazoezi au mchezo. 

 

  1. Huongeza ufanisi wa Mchezaji Uwanjani. Massage kabla ya mchezo humpa nguvu mchezaji, kumuongezea molari na kumuondolea msongo wa mawazo, hivyo mchezaji huwa huru na anategemewa zaidi kuonyesha ufanisi mkubwa kuliko yule asiyefanyiwaa massage ya mchezo. Mwanamichezo Paavo Nurmi mwanariadha maarufu wa Finland alikuwa anafanya massage na ikapelekea kushinda taji mara tano mfululizo mnamo mwaka 1924.

 

  1. Huzuia hatari ya kupata jeraha mchezoni. Massage huondoa mkazo wa misuli (muscles tention) na hulainisha tishu za misuli hivyo huzuia hatari ya kupata jeraha mchezoni. Pia huzuia kuvimba sehemu zinazogongwa wakati mwanamichezo akiwa mchezoni.

 

  1. Huondoa uchovu baada ya mchezo. Baada ya misuli kufanya kazi kwa kitambo fulani huchoka, kuchoka kwa misuli hupelekea pia kuchoka kwa mwili wote hivyo, Massage ya michezo huwasaidia wanamichezo kupumzika mara mbili zaidi ya kupumzika kwa kawaida. Hii ni kwa sababu massage huzalisha endorphin hormone ambayo huleta furaha kwa mtu.

 

  1. Husaidia kubadili sumu katika misuli kuwa nishati. Baada ya misuli kufanya kazi katika mchezo kiasi kikubwa cha lactic acid hujirundika katika seli za misuli. Tafiti zilizofanywa hivi karibuni zimeonyesha kuwa kiasi hicho cha lactic acid ambacho ni sumu kina uwezo wa kubadilishwa na kuwa nishati baada ya kufanyiwa massage.

 

  1. Huboresha mjongeo wa viungo (joint movements). Massage ya Michezo husaidia pia kuboresha mjongeo wa viungo hivyo kumfanya mwanamichezo kukimbia au kuruka kwa urahisi zaidi akiwa katika mchezo.

 

Hivyo inashauriwa kwa mwanamichezo kupata huduma ya massage mara kwa mara kwa ajili ya kuuweka fiti mwili wake na kuongeza ufanisi maradufu katika mchezo.

 

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Scroll to Top